Uongozi wa klabu ya Young Africans umekamilisha taratibu za kumsajili aliyekua mshambuliaji wa pembeni wa Alliance FC ya jijini Mwanza, David Richard, kwa mkataba wa miaka miwili.
Richard ambaye msimu huu uliomalizika amefunga mabao manane, anatua Young Africans akiwa mchezaji huru baada ya mkataba wake na Alliance FC iliyoshuka daraja msimu huu kumalizika.
Nyota huyo ambaye aliifungia Alliance hat-trick katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Mwadui FC, wakati wakishinda mabao manne kwa moja, mabao hayo akifunga dakika ya tano, 18 na 83 huku lile la nne likifungwa na Sameer Vicent, anakuwa mchezaji wa tano kusajiliwa na Young Africans katika dirisha hili.
Wachezaji wengine ambao tayari Young Africans imewasajili tangu kufunguliwa kwa dirisha Agosti Mosi, ni pamoja na mshambuliaji Wazir Junior kutoka Mbao FC, beki wa kati Bakari Mwamnyeto aliyekuwa akikipiga Coastal Union, Zawadi Mauya kutoka Kagera Sugar na Yasin Mustapha wa Polisi Tanzania.
Taarifa nyingine zinaeleza kuwa klabu ya Young ipo katika mpango wa kumnasa kiungo wa Azam FC, Salim Abubakar ‘Sure Boy’, ambaye ametajwa kuingia kwenye rada za klabu hiyo.
Juzi klabu hiyo kongwe nchini ilitangaza kubaki na wachezaji 15 tu kati ya 29 wa kikosi cha msimu uliopita, hivyo 14 kufunguliwa mlango wa kutokea kwa sababu mbalimbali ikiwamo mikataba yao kumalizika na kutohitaji tena huduma zao na baadhi viwango kushuka, wachezaji hao ni pamoja na nahodha Papy Tshishimbi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Wengine ni David Molinga ‘Falcao, ambaye naye anatokea DRC na wazawa Jaffary Mohamed, Tariq Seif, Andrew Vincent ‘Dante’, Mohamed Banka, Mrisho Ngassa, Ally Mtoni ‘Sonso’, Muharami Issa ‘Marcelo’, Ali Ali, Muivory Coast Yikpe Gislain, Mnyarwanda Patrick Sibomana, Mzambia Erick Kabamba na Raphael Daudi.
Akizungumzia kasi ya mafuriko hayo ya usajili, Afisa Habari wa Young Africans, Hassan Bumbuli, amesema hatua wanazochukua katika kukisuka upya kikosi cha timu hiyo ni kwa sababu ya kiufundi na si mihemko ya mashabiki au wachambuzi wa soka nchini, lakini pia akaahidi sasa wanageukia nyota wapya wakuja na ndege (kutoka nje) kusajiliwa.
Bumbuli amesema baada ya kutangaza majina ya wachezaji walioachwa kumekuwa na maneno mengi ya pembeni yakibeza hatua waliyochukua viongozi huku wakihoji usajili huo unafanywa na nani wakati timu haina kocha, jambo ambalo alidai klabu hiyo ina kamati ya ufundi, lakini pia Mwenyekiti wao, Dk. Mshindo Msolla kitaaluma ni kocha.
“Tupo kwa ajili ya kujenga timu na si kubomoa, hatua ambazo zinachukuliwa na uongozi ni thabiti kwa ajili ya kukiimarisha kikosi chetu kuelekea msimu mpya, mchezaji ambaye ameachwa ama kubakishwa kikosini zipo sababu za kufanya hivyo, uongozi haufanyi kazi kwa mihemko ingawa tunajua Wanayanga wanataka furaha baada ya kuona tumekosa ubingwa msimu huu,” alisema.
Kuhusu Tshishimbi, Bumbuli amesema amefika makubaliano na uongozi huku kila upande ukiridhika kuachana baada ya kushindwa kukubaliana dau.