Klabu ya Young Africans imeshauriwa kufanya kweli kama wanahitaji huduma ya mshambuliaji wa FC Saint-Éloi Lupopo ya DR Congo, Mpiana Mozizi kuelekea msimu ujao wa ligi kuu ya soka Tanzania bara.
Ushauri huo kwa Young Africans umetolewa na kocha wa zamani wa FC Saint-Éloi Lupopo ambaye kwa sasa ni kocha mzaidi wa As Vita Raoul Shungu, ambapo amesema kama hesabu za klabu hiyo ni kweli zimeangukiwa kwa Mozizi, wanapaswa kufanya hima ili kukamilisha mipango yao.
Shungu ambaye aliwahi kukinoa kikosi cha Young Africans miaka iliyopita, amesema Mozizi ni mshambuliaji bora na ana vigezo vyote vya kuitumikia klabu hiyo yenye maskani yake makuu kwenye makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani jijini Dar es salaam.
“Huyu ni mshambuliaji mzuri sana nasikia hayo maneno, pia naona kwenye vyombo vya habari huko Tanzania, Young Africans wanamtaka Mozizi,” alisema Shungu.
“Mozizi hapa DR Congo ndio anaongoza kwa kufunga mabao anafunga sawa na mchezaji wetu Fiston (Mayele) na Muleka (Jackson) wa TP Mazembe hao wote wanafunga idadi sawa.”
Akimchambua kwa ubora wake, Shungu alisema Mozizi anaijua kazi yake ya kufunga na wala sio mshambuliaji mwepesi kukabika kutokana na kiu yake ya kutamani kufunga kila mchezo.
Kocha huyo msaidizi wa AS Vita inayoongozwa na Florent Ibenge alisema Mozizi anajua kufunga kwa kichwa na hata miguu lakini pia ana nguvu sana.
“Hapo Tanzania watu wanataka mchezaji kama Mozizi ana nguvu sana hakati tamaa anafunga kwa miguu na hata kichwa na beki akimsahau au akafanya makosa kidogo tu ameumia atakuwa ameshafunga.”
“Young Africans nawajua na mpira wao, kama wana mawinga wazuri na hata viungo wengine wanaojua kumpa nafasi atawafanyia kazi kubwa sana.”
Young Africans wanabahati ya kupata wachezaji wazuri kutoka hapa lakini pia wana viongozi ambao hapa DR Congo wanaheshima kubwa, kwa hiyo sioni kama watapata shida kumpata Mozizi,” alisema Shungu.
“Hata wachezaji wa hapa wanapenda kuchezea timu zenye mashabiki wengi kama Young Africans au Simba, kama Young Africans watampata watafurahia na hata Mozizi mwenyewe akifanya vizuri atafurahia maisha ya hapo, Tanzania kuna mashabiki wengi wanapenda timu zao sana,” aliongeza Kocha huyo anayezungumza kiswahili kizuri.