Uongozi wa Young Africans umeandaa mikakati ya kusherehekea ubingwa wa 26 wa Ligi Kuu Bara baada ya kurejea toka nchini Angola watakakokwenda kucheza mechi ya marudiano dhidi ya G.D Sagrada Esperanca Jumatano ijayo.

Young Africans imetawazwa kuwa mabingwa wa ligi hiyo baada ya kufikisha pointi 71 ambazo hakuna timu yoyote itakayoweza kuzifikia na kuweza kunyakua kombe hilo kwa mara ya pili mfululizo.

Afisa habari wa klabu hiyo, Jerry Muro amewataka wanachama wa klabu hiyo kujitokeza kwa wingi keshokutwa Jumamosi katika Uwanja wa Taifa katika mchezo wao dhidi ya Ndanda FC utakaotumika kukabidhiwa kombe la ubingwa huo.

Mchezo huo ulitakiwa ufanyike Nangwanda Sijaona mjini Mtwara lakini kutokana na mabingwa hao kubanwa na ratiba ya Kombe la Shirikisho barani Afrika waliamua kukaa meza moja na wenzao kujadili kuhamisha mechi hiyo na kufikia makubaliano ya kucheza hapa jijini Dar es Salaam.

“Tulipeleka hoja kwa wenzetu Ndanda kuhusu ratiba yetu ya Kombe la Shirikisho, tunashukuru wametuelewa na kuonesha uzalendo kwa nchi ambayo itasaidia kuwapa maandalizi katika mchezo wetu na Sagrada,” alisema Muro.

Akizungumzia mchezo huo wa marudiano, Muro alisema timu itasafiri  Jumapili baada ya mchezo wao dhidi ya Ndanda. Katika mchezo wa awali Young Africans waliwafunga wapinzani wao bao 2-0, mchezo uliofanyika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Tottenham Hotspurs Wazima Ndoto Za Man Utd
Watanzania Kusimamia Sheria 17 Za Soka Ethiopia Vs Ghana