Idara ya Habari na Mawasilino ya Young Africans imewatoa wasiwasi Wanachama na Mashabiki wa klabu hiyo kuhusu kikosi chao, baada ya kuwasili Jijini Mwanza jana Ijumaa (Machi 04), kikitokea Dar es salaam.

Young Africans ipo jijini Mwanza, kwa ajili ya mpambano wa Ligi Kuu Tanzania Bara Mzunguuko wa 17 dhidi ya Geita Gold FC, utakaopigwa Uwanja wa CCM Kirumba kesho Jumapili (Machi 06).

Mkuu wa Idara hiyo Hassan Bumbuli, amesema kikosi chao kipo katika hali nzuri na kina ari kubwa ya kupambana kesho Jumapili (Machi 06) na kuendelea kupata matokeo mazuri ambayo yatawafanya kung’ang’ania kileleni mwa Msimamo wa Ligi Kuu.

“Timu yetu imejipanga vizuri kuelekea katika mchezo huo, tunaomba mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi katiak Uwanja wa CCM Kirumba, tuko tayari kwa mapambano,” amesema Bumbuli.

Wakati huo huo Kocha Msaidizi wa Young Africans Cedrick Kaze amesema wachezaji wake wako katika hali nzuri na kila mmoja anahitaji kuona wanaendeleza kasi ya ushindi waliyonayo msimu huu.

Amesema mchezo huo utakuwa mgumu kwa sababu msimu huu kila timu imejipanga vizuri na inahitaji kujiepusha na janga la kushuka daraja.

“Tunakwenda kukutana na timu ya Geita Gold, lengo leti katika mechi hiyo ni kupata matokeo mazuri na kujiimarisha kwenye mbio za ubingwa,” alisema Kaze.

“Hali za wachezaji ambao walikuwa majeruhi zinaendelea vizuri, baadhi yao wanakaribia kurejea kikosini na kilichobaki ni kusubiri taarifa kutoka kwa daktari wa timu ili kufahamu tutakaowakosa,” amesema Kaze

Ligi Kuu Bara inatarajia kuendelea tena leo Jumamosi (Machi 05) kwa mchezo kati ya Azam FC dhidi ya Polisi Tanzania kwenye Uwanja wa Azam Complex huku kesho Jumapili (Machi 06) Ruvu Shooting ikiwaalika Biashara United, Coastal Union ikiwafata KMC na Simba ikiwaalika Dodoma Jiji FC keshokutwa Jumatatu (Machi 07).

Waamuzi Ligi Kuu wapewa KONGOLE
Putin aonya vikwazo vya kimataifa vitakwakasirisha