Majuma mawili kabla ya mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika kati ya Mabingwa wa Soka nchini Nigeria Rivers United dhidi ya Mabingwa wa Tanzania Bara Young Africans, Benchi la Ufundi la Wananchi limeweka wazi ratiba ya mazoezi makali ambayo yatasaidia kuendeleza moto katika michuano ya kimataifa msimu huu 2022/23.
Licha ya matarajio ya kupambana na Geita Gold FC leo Jumamosi (April 08) katika Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es salaam, Benchi la Ufundi la Young Africans linaamini lina kazi kubwa ya kuhakikisha wanaizaimisha Rivers United katika mchezo wa Robo Fainali, ambao utaanzia ugenini katika Uwanja wa Adokiye Amiesimaka uliopo katika mji wa Port Horcout, Rivers nchini Nigeria, huku mchezo wa pili ukipangwa kupigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam April 30.
Kocha Msaidizi wa Young Africans, Cedric Kaze amesema wana kila sababu ya kujiandaa vizuri kabla ya kwenda kupambana Rivers United, kwa sababu wanatambua ni timu nzuri na yenye uwezo wa kupambana nyumbani na ugenini.
Amesema kikosi chao kimekuwa na maandalizi ya kuelekea mchezo wa Kombe la ASFC dhidi ya Geita Gold na baadae kitaendelea kujiwinda na mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar kabla ya kucheza na Simba SC April 16 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, hivyo wanaamini kila hatua ya maandalizi yao itawajenga kuelekea mchezo huo wa Kimataifa.
“Tumepangwa kucheza dhidi ya Rivers United katika ratiba ya michezo yetu miwili ya Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kwa kuwa tunataka kuhakikisha tunafuzu hatua ya Nusu Fainali, tayari tumeanza maandalizi awali ya mchezo ya huo.”
“Tuna ratiba ya michezo ya mashindano ya ndani lakini tunafahamu mchezo dhidi ya Rivers hauko mbali hivyo tunatarajia kuanza mara moja program ya kujiandaa na mcheza huo mara tu, tutakapomalizana na ratiba ya mchezo wetu dhidi ya Geita Gold.”
“Tutacheza na Kagera Sugar na kisha Simba SC, kwa hiyo michezo yote hii itakuwa sehemu ya maandalizi yetu kabla ya kukutana na Rivers United, ninaamini tutakuwa na maandalizi mazuri na tutapambana kwa lengo la kupata matokeo mazuri.” Amesema Kaze