Klabu ya Young Africans imeshukuru kuikwepa klabu ya Pamba FC katika michuano ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’, baada ya kupangwa kwa Ratiba ya Hatua ya Robo Fainali jana Jumatatu (Februari 21).
TFF kwa kushirikiana na Wadhamini Wakuu wa Michuano hiyo Kampuni ya Azam Media ilipanga Ratiba ya Robo Fainali ya ‘ASFC’, huku Young Africans ikiangukia mikononi mwa Geita Gold FC inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Young Africans Hassan Bumbuli amesema baada ya kufanikiwa kuwa sehemu ya klabu zilizotinga Hatua ya Robo Fainali ya ‘ASFC’ walikua wakiomba wasipangwe kukutana na Pamba FC inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara.
Amesema Pamba FC ni klabu inayocheza katika Daraja tofauti na ilipo klabu yao kwa sasa, hivyo ingekua vigumu kuisoma namna inavyocheza na huenda ingewapa wakati mgumu kupambana nayo kwenye hatua hiyo.
“Tunashukuru hatukupangiwa kucheza dhidi ya Pamba FC, tunajua hii ni timu ya Ligi Daraja la Kwanza, tunaamini ingetusumbua sana katika kufikia malengo yetu ya kulisaka taji hili, nawapa pole kwa waliokutanishwa na hawa jamaa.”
“Timu ya Geita Gold ni Levo yetu na tunaimudu kwa sababu inacheza katika Daraja tulilopo sisi Young Africans, hivyo tunaamini tutaweza kuisoma kulingana na itakavyokua ikibadilika kabla ya mchezo wetu wa Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho.” Amesema Bumbuli.
Michezo mingine ya Robo Fainali iliyopangwa jana Jumatatu (Februari 21), Mabingwa watetezi Simba SC wameangukia mikononi mwa Pamba FC, Azam FC imepangwa kucheza dhidi ya Polisi Tanzania huku Coastal Union ikipangwa kukutana na Kagera Sugar.