Vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara Young Africans wamesema watacheza kwa heshima zote dhidi ya Tanzania Prisons katika mchezo wa leo Jumatatu (Mei 09), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Young Africans itaingia dimbani ikiwa na kumbukumbu ya matokeo ya sare ya bila kufungana dhidi Ruvu Shooting, walioyapata mjini Kigoma Uwanja wa Lake Tanganyika Jumatano (Mei 04).
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Klabu hiyo Kongwe katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati Hassan Bumbuli amesema, hatua ya kuendelea kuongoza msimamo wa Ligi katu hauwezi kuwafanya wakawa na dharau na timu nyingine kama Tanzania Prisons inayoshika nafasi za chini.
Amesema dhamira yao ya kila mchezo ni Fainali wanaendele nayo, na wana uhakika itawasaidia katika mpambano wa leo, ambapo wanahitajika kupata matokeo yatakayowapa alama tatu muhimu.
“Hatutaidharau Tanzania Prisons, ni timu inayoshiriki Ligi Kuu na tunaamini ina uwezo mkubwa licha ya kuwa katika nafasi za chini, tupo katika daraja moja na hatupaswi kabisa kuona tunacheza na timu ya kawaida kwa kigezo cha matokeo walioyapata siku za nyuma.”
“Wachezaji wetu wameshaambiwa hilo, na wanajua nini cha kufanya watakapokua Uwanjani baadae jioni leo, hata kwa mashabiki wetu nao wanapaswa kuiheshimu Tanzania Prisons, waipe heshima kubwa kama walivyowahi kutoa heshima kwa timu nyingine tulizocheza nazo msimu huu.”
“Tunajua Tanzania Prisons, itahitaji kushinda mchezo wa leo ili kujiondoa katika nafasi mbaya waliopo sasa, na hapo ndipo kwenye mtihani mzito wa kupambana nao.” amesema Hassan Bumbuli.
Tanzania Prisons ilipoteza mchezo uliopita kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Mbeya Kwanza FC mjini Songea mkoani Ruvuma juma lililopita, hivyo itautumia mchezo wa Young Africans kama sehemu ya kutaka kurekebisha makosa.
Klabu hiyo inayomilikiwa na Jeshi la Magereza Tanzania, inashika nafasi ya 15 ikiwa na alama 22, huku Young Africans ikiwa kileleni kwa kuwa na alama 56.