Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans wamesema wamejipanga kucheza ‘kikubwa’ katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wenyeji Rivers United itakayochezwa keshokutwa Jumapili (April 23) kwenye Uwanja wa Godswill Akpabio, Nigeria.
Kikosi cha Young Africans chenye wachezaji 24, kilichoweka kambi fupi jijini Lagos, leo asubuhi kilitarajiwa kuanza safari ya kuelekea katika Mji wa Uru tayari kwa mtan- ange huo.
Afisa Habari wa Young Africans, Ali Kamwe amesema wanajua mechi hiyo itakuwa ngumu, lakini wataicheza kikubwa ili kufanya mchezo wa marudiano utakaochezwa hapa nchini wiki ijayo kuwa rahisi.
Kamwe amesema Young Africans inajipanga kuhakikisha inapata ushindi na kujiondoa na janga la kufungwa idadi kubwa ya mabao ili kujiweka kwenye nafasi salama ya kuwania kusonga mbele.
“Watanzania wengi tunaamini timu zikija kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, kuna asilimia kubwa ya kushinda, lakini siku zote wakati mwingine mpira hauko hivyo, katika mechi hizi za mtoano kama hautocheza vizuri ugenini bado utakuwa na matatizo ukicheza nyumbani, sisi Yanga hatutamani kufikia huko, yaani tuwe na mlima wa kusawazisha mabao matano hapa,”amesema Kamwe.
Afisa huyo amesema wachezaji wote waliocheza mechi ya ‘dabi’ wako vizuri na wa nashukuru mchezo huo haukuzalisha majeruhi, hivyo kila mmoja yuko tayari kuipamba- nia klabu.
Alikiri wanafahamu haitakuwa kazi rahisi kuwakabili wapinzani wao kwa sababu ya rekodi nzuri waliyonayo wanapocheza nyumbani kwao.
“Tunajua Rivers United ni timu nzuri hasa ikiwa kwao, kwa mujibu wa rekodi zinavyoonyesha hivyo, hata Wydad Casablaca ilifungwa mabao 2-1 ilipokwenda kucheza huko katika hatua za mwanzo za Ligi ya Mabingwa Afrika, ingawa ilitolewa lakini bado rekodi yake inabaki pale pale, ni wagumu mno kwao.”
“Sisi tumeshalijua hilo, ndiyo maana ninasema tunakwenda kucheza kikubwa, na mechi nzuri zaidi itachezwa ugenini,” amesema Ally Kamwe
Wakati Young Africans inaongoza katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 68, Rivers United inashika nafasi ya pili kwenye Kundi B, ikiwa na alama 23, ikizidiwa na kinara Lobi Stars yenye alama 26. Kundi A katika Ligi Kuu Nigeria linaongozwa na Bendel yenye alama 28.
Mabingwa hao watetezi pia wa mashindano ya Kombe la FA watashuka dimbani wakiwa na maumivu ya kufungwa mabao 2-0 na watani zao, Simba SC katika mechi ya marudiano ya Ligi Kuu Tanzania Bara.