Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans umekanusha taarifa zinazomuhusu Beki wa Kushoto kutoka DR Congo Joyce Lomalisa Mutambala kuwa njiani kuondoka klabuni hapo katika kipindi hiki cha usajili wa Dirisha Kubwa.
Lomalisa amekuwa akiripotiwa kuushinikiza Uongozi wa Young Africans kwa njia ya Barua akiutaka kumuachia ili aondoke na kwenda kusaka maisha mahala pengine, kutokana na kushindwa kucheza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza, huku nafasi yake ikichukuliwa na Beki mzawa Kibwana Shomari.
Uongozi wa klabu hiyo umesema mchezaji huyo hataondoki klabuni hapo kwa kuwa wana mkataba naye wa mwaka mmoja zaidi na hakuna ofa yoyote ya kutaka kumsajili iliyowasilishwa klabuni hapo.
Afisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe amesema taarifa zinazosema kuwa mchezaji huyo ameomba kuondoka au anaondoka si za kweli, hivyo kuwatoa hofu Wanachama na Mashabiki wa timu hiyo.
“Kuna taarifa zinaanzishwa kwa ajili ya kutaka kuvuruga utulivu wetu, kwa mlengo wa kibiashara, au mawakala wanatengeneza tu ili wachezaji wao wajadiliwe kupata mikataba mikubwa zaidi, Lomalisa ni mchezaji wetu halali amebakisha mkataba wa mwaka mmoja, na kama hawa wachezaji wote wa Young Africans wenye mikataba watataka kuondoka kwenye klabu yetu, maana yake ni lazima wafuate taratibu ambazo viongozi wa Yanga ni lazima wakae chini waziangalie ofa,” amesema Kamwe.
Kamwe amewataka Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo kuwa watulivu hasa kipindi hiki cha usajili ambapo watasikia mengi yanayowahusu wachezaji wo kwa sababu wamefanya vyema kwenye michuano ya kimataifa.
“Kwanza niwaambie wanachama na mashabiki wa Young Africans kuwa tupo kwenye kipindi cha usajili, kipindi hiki kina habari nyingi kweli kweli, kuna tetesi nyingi sana, muhimu ni kuamini tu yale ambayo viongozi wao tutayasema kupitia vyanzo rasmi vya klabu au kupitia mahojiano tunayoyafanya na vyombo vya habari wakisikia tunazungumza, Young Africans ni klabu kubwa hivi sasa ndiyo maana wachezaji wetu kila siku wanahusishwa kuondoka kwenye klabu yetu,” amesema Kamwe.