Uongozi wa Klabu ya Young Africans umetoa ufafanuzi wa Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Uganda Milutin Sredojević ‘Micho’, baada ya kuonekana Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, akifuatilia mchezo wao dhidi ya Simba SC jana Jumapili (Oktoba 23).
‘Micho’ ambaye aliwahi kukinoa kikosi cha Young Africans mwaka 2007, alifuatilia mchezo huo uliomalizika kwa sare ya 1-1, huku Simba SC wakitangulia kupata bao kupitia kwa Augutine Okrah, kabla ya Stephen Aziz Ki kuwasazishia wenyeji sekunde chache kabla ya mapumziko.
Afisa Habari wa Young Africans Ally Kamwe amezungumza na Dar24 Media katika mahojiano maalum na kueleza kuwa, ujio wa Kocha ‘Micho’ ulikua wa kawaida na wala hauna uhusino wowote na tetesi zinazoendelea katika Mitandao ya Kijamii.
“Ujio wa Kocha Micho ni kama ilivyokua kwa Pitso, alikuja kuangalia Dabi na tulimkaribisha kama mwanafamilia, kwa hiyo hakuna lolote linaloendelea kati ya Klabu na Kocha huyo.”
“Tunamuheshimu na tunampenda na ndio maana alivyotuambia anakuja kuangalia mchezo wetu, tulijiandaa kumpokea na tulifanya hivyo hadi mlipomuona Uwanjani akifuatilia mchezo wetu na Simba SC.” amesema Ally Kamwe
Hata hivyo alipoulizwa Kocha Micho baada ya mchezo huo, aliwaambia Waandishi wa Habari kuwa alikuja Tanzania kwa ajili ya kuangalia Kariakoo Dabi, na hakuna lolote linaloendelea kati yake na Uongozi wa Young Africans.
“Hapana, mimi bado Kocha wa Uganda ‘The Cranes’ na ninafanya kazi yangu.” alisema Micho alipozungumza na waandishi wa habari.
Awali Micho alihusishwa na mpango wa kuwa kwenye mazungumzo na Uongozi wa Young Africans ili kuchukua nafasi ya Kocha Nasreddine Nabi, ambaye kabla ya mchezo dhidi ya Simba SC alitabiriwa huenda ngetimuliwa kazi.