Young Africans imefikisha alama 9 katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kuifunga KMC FC mabao 2-0 leo Jumanne (Oktoba 19) mjini Songea mkoani Ruvuma.
Mchezo huo wa mzunguuko wa tatu wa Ligi Kuu msimu wa 2021/22 umechezwa kwenye Uwanja wa Majimaji, ambao kwa leo ulikua nyumbani kwa KMC FC.
Mabao ya Young Afticans yamepatikana kipindi cha kwanza dakika ya 06 na 11 kupitia kwa Mshambuliaji kutoka DR Congo Fiston Mayele na Kiungo kutoka Zanzibar, Tanzania Feisal Salum.
Hata hivyo umahiri wa safu ya kiungo ya Young Africans iliyokua inaratibiwa Khalid Aucho Yanick Bangala na Feisal Salum ndio ilikua chachu ya upatikanaji wa mabao hayo ya ushindi.
Kipindi cha pili KMC FC ilionesha kuamka na kulisakama lango la Young Africans lakini kukosa umakini wa pasi za mwisho uliwanyima kukwamisha mpira wavuni katika lango la wageni wao.
Kupoteza kwa KMC FC kunaendelea kuifanya klabu hiyo ya Kinondoni jijini Dar es salaam kusalia na alama moja baada ya kushuka dimbani mara tatu, huku ikiburuza mkia katika msimamo wa Ligi Kuu.
Alama 9 za Young Africans zinaipaisha klabu hiyo kongwe nchini hadi kwenye nafasi ya kwanza katika msimamo wa Ligi Kuu.