Kikosi cha Vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara Young Africans kimewasili salama Jijini Mwanza kikitokea Dar es salaam leo Ijumaa (Machi 04).
Young Africans keshokutwa Jumapili (Machi 06) itacheza mchezo wa Mzunguuko wa 17 wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Geita Gold FC, Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza saa Kumi jioni.
Young Africans imeondoka na asilimi kubwa ya wachezaji wake mahiri kuelekea mchezo huo, ambao unatarajiwa kuwa sehemu ya burudani ya mwishoni mwa juma kwa wakazi wa Jiji la Mwanza na maeneo ya karibu.
Gaita Gold ambao watakua wenyeji wa mchezo huo, wamelazimika kuchagua Uwanja wa CCM Kirumba kutokana na Uwanja wao wa nyumbani wa Shule ya Sekondari ya Nyankungu kutokua na Uwezo wa kuchukua mashabiki wengi ambao wanatarajiwa kushuhudia mchezo wao dhidi ya Young Africans.
Katika mchezo wa Duru la Kwanza la Ligi Kuu msimu huu uliozikutanisha timu hizo uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, Young Africans ilichomoza na ushindi wa bao 1-0, lililofungwa na Kiungo Mshambuliaji Jesus Moloko.
Young Africans inaendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 42, huku Geita Gold FC yenye matokeo ya mazuri kwa siku za karibuni ikiwa na alama 21 zinazoiweka katika nafasi ya 07 kwenye msimamo.