Baada ya kukamilisha vyema majukumu ya kimataifa kwa kutinga hatua ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kikosi cha Young Africans kesho Jumatano (Oktoba 04) kinatarajia kushuka Uwanja wa Highland Estate, Mbarali mkoani Mbeya kucheza na Ihefu FC ikiwa ni mchezo wa raundi ya nne wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Meneja wa timu hiyo, Walter Harison amesema kikosi chao kimeelekea Mbeya leo Jumanne (Oktoba 03) kwa ajili ya mchezo huo ambao wanaamini utakuwa na ushindani mkubwa kutokana na uchovu waliokuwa nao wachezaji wao.

“Timu imeondoa leo kuelekea Mbeya tukiwa na kikosi kamili sababu baada ya Mbeya tutakwenda Mwanza kucheza na Geita, kiujumla lengo letu katika mechi zote hizi ni kupata pointi tatu ingawa tunatarajia kupata upinzani mkali kwa sababu ya uchovu waliokuwa nao wachezaji wetu kutokana na kukosa muda wa kupumzika,” amesema Walter.

Meneja huyo amesema uchovu wa wachezaji wao unatokana na ufinyu wa ratiba ambao umesababisha wachezaji kukosa muda wa kupumzika lakini pia kufanya mazoezi ya kutosha kujiandaa na mchezo unaofuata lakini watapambana nalo kama ratiba inavyowaelekeza.

Amesema kocha wao wa viungo, Taibi Lagrouni kwa sasa anafanya kazi kubwa ya kuhakikisha wachezaji wao wanakuwa katika hali nzuri ya upambanaji kuipigania timu yao kupata ushindi katika mashindano yote yanayowakabili.

Walter amesema upana wa kikosi chao pia umekuwa msaada mkubwa kwa Kocha wao mkuu, Miguel Gamondi ambaye amekuwa akibadili kikosi chake katika mechi tofauti jambo ambalo linasaidia timu yao kucheza kwa uwiano mzuri kila mechi.

Young Africans ipo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu, ikikusanya pointi 9 baada ya kushinda mechi zote tatu ilizocheza hadi sasa na kufunga mabao 11 huku ikiwa haijaruhusu bao kwenye wavu wake.

Victor Osimhen avunja ukimya SSC Napoli
Azam FC kuishusha Young Africans kileleni?