Uongozi wa Young Africans una matumaini ya kupata ushindi kwenye mchezo ujao wa Ligi Kuu dhidi ya Matibwa Sugar, utakaochezwa Jumapili, Septemba 27 kwenye uwanja wa Jamuhuri mjini Morogoro.

Young Africans tayari wameondoka jijini Dar es salaam kuelekea mkoani Morogoro kwa ajili ya mpambano huo, unaosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini, kutokana na timu hizo kuwa na upinzani mkali kila zinapokutana, hususan kwenye Uwanja wa Jamuhuri.

Makamu Mwenyekiti wa Klabu hiyo, Frederick Mwakalebela, amesema anaamini kikosi kitapambana vilivyo kwenye mchezo huo, kufuatia maandalizi mazuri yanayoendelea kufanywa na benchi la ufundi linaloongozwa na Kocha Zlatko Krmpotic.

Mwakalebela amesema wachezaji wote wapo katika hali nzuri na wana morari ya kuridhisha kuelekea mpambano dhidi ya Mtibwa Sugar.

“Wachezaji wote wanaendelea vizuri, leo alfajiri tulianza safari kuelekea mjini Morogoro kujiandaa kukutana na  Mtibwa Sugar wikiendi hii, maandalizi kwa ajili ya mchezo huo yatakamilishwa ndani ya siku mbili hizi.” amesema Mwakalebela.

Mchezo uliopita, Young Africans ikiwa ugenini kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, iliibuka na alama tatu baada ya kushinda kwa bao moja kwa sifuri dhidi ya wenyeji wao Kagera Sugar, huo ukiwa ni ushindi wa pili mfululizo ikishinda kwa bao moja baada ya kuichapa Mbeya City katika dimba la Mkapa jijini Dar es Salaam.

Lakini katika mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu msimu huu dhidi ya Tanzania Prisons, ililazimishwa sare ya bao moja kwa moja katika Uwanja wa Mkapa.

Lowassa alivyomtumia ujumbe JPM, ‘inatisha lakini usitishike’
Watanzania zaidi ya 150,000 kufaidika na mradi wa boresha macho