Kikosi cha Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans kimewasili salama mkoani Mtwara tayari wa safari ya kuelekea Lindi ambako kitacheza dhidi ya Namungo FC.
Young Africans itakua mgeni katika mchezo huo wa Mzunguuko wa 15 wa Ligi Kuu, ambao umepangwa kuunguruma keshokutwa Jumatano (Desemba 07) katika Uwanja wa Majaliwa mjini Ruangwa.
Baada ya kuwasili mkoani Mtwara kikosi cha Young Africans kilipata mapokezi kutoka mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo Kongwe katika Ukanda wa Afrika Mashariki.
Young Africans imesafiri kuelekea Lindi, saa chache baada ya kucheza mchezo wa Ligi Kuu mzunguuko wa 14 dhidi ya Tanzania Prisons jijini Dar es salaam na kuibuka na ushindi wa 1-0, bao ambalo lilifungwa na Kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’.
Ushindi dhidi ya Tanzania Prisons umeifanya Young Africans kufikisha alama 35, ikifuatiwa na Simba SC yenye alama 34, huku Azam FC ikiendelea kuwa na alama 32.
Azam FC itacheza mchezo wake wa 15 leo Jumatatu (Desemba 05) dhidi ya Polisi Tanzania mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro katika Uwanja wa Ushirika.