Kocha msaidizi wa Young Africans Cedrick Kaze amesema nguvu na mawazo wamevigeuzia katika mchezo wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’, huku akijizatiti kutetea ubingwa wa michuano hiyo.
Young Africans itacheza dhidi ya Geita Gold FC Jumamosi (April 08) katika Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es salaam, ikiwa na lengo la kusaka nafasi ya kutinga Nusu Fainali ya ‘ASFC’ kwa mara ya pili mfululizo.
Kocha Kaze amesema baada ya kikosi cha Young Africans kurejea jijini Dar es salaam jana Jumatatu (April 03) kikitokea Lubumbashi DR Congo, ambako kilikuwa na mchezo wa mwisho wa Kundi D, Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya TP Mazembe, mara moja kinaanza mazoezi ya kujiwinda na mchezo dhidi ya Geita Gold FC.
Kocha huyo amesema lengo kubwa ni kuhakikisha wanashinda mchezo huo, ili kuendelea kuishi katika malengo waliojiwekea msimu huu 2022/23, hivyo ana uhakika maandalizi yatakayofanya yatatosha kuisambaratisha Geita Gold FC Jumamosi (April 08).
“Tunatarajia upinzani kutoka kwa Geita, kwa sababu tunafahamu wana kikosi kizuri ambacho kimetupa upinznai mkubwa katika michezo ya Ligi Kuu msimu huu, tunakwenda kuanza maandalizi ya kujiandaa na mchezo huo wa Jumamosi.”
“Lengo letu kubwa ni kuendelea kuishi katika malengo yetu tuliojiwekea msimu huu, kwa kuhakikisha tunatwaa ubingwa wa michuano yote tunayoshiriki, kwa hiyo tumejipanga kufanikisha kila hatua tunayoipitia.” Amesema Kaze
Kikosi cha Young Africans kiliwasili jijini Dar es salaam jana jioni, kikitokea Lubumbashi DR Congo ambako kiliacha maumivu kwa TP Mazembe iliyokubali kulala kwa bao 1-0 katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika, uliopigwa Uwanja wa Tp Mazembe Jumapili (April 02).