Uongozi wa Young Africans umetangaza rasmi vita dhidi ya Mbeya Kwanza FC, baada ya kumalizana na Dodoma Jiji FC jana Jumapili (Mei 15), mjini Dodoma katika Uwanja wa Jamhuri.
Katika mchezo huo Young Africans ilichomozana ushindi wa mabao 2-0, yaliyofungwa na Dickson Ambundo na Mohamed Yusuph aliyejifunga.
Makamu Mwenyekiti Wa Kamati Ya Usajili ya Young Africans Eng.Hersi Said amesema wamejipanga kukusanya alama tatu za mchezo mmoja baada ya mwingine, hivyo Mbeya Kwanza FC wanapaswa kujiandaa, kwani wao ndio wanafuata kwa mujibu wa Ratiba ya Ligi Kuu.
“Malengo yetu sisi ni kutwaa ubingwa lakini ubigwa hauji hivi hivi, ni lazima tupambane katika michezo iliyosalia, hivyo tutahakikisha tunashinda mchezo mmoja baada ya mwingine.”
“Tutahakikisha tunashinda mchezo wetu dhidi ya Mbeya kwanza FC tarehe 21 mwezi huu, tunajua umuhimu wa mchezo huo na alama zake, na ndio maana tumetangaza mapema, tunahitaji kushinda ili tufikie lengo la kuwa mabingwa msimu huu.”
“Tumebakiza michezo sita, katika hii michezo sita tukiweza kukusanya alama 11 tunaweza kuwa katika nafasi ya kuchukua ubingwa mapema zaidi, kwa hiyo kwetu sisi malengo ni kuchukua ubingwa.”
Young Africans inaelekea kwenye mchezo wa Mzunguuko wa 25 ikiendelea kuwa kileleni kwa kufikisha alama 60, huku mpinzani wake mtarajiwa Mbeya Kwanza FC akiburuza mkia kwa kuwa na alama 21 zilizopatikana katika michezo 22.