Licha ya Young Africans kukubali kumuuza Kiungo Mshambuliaji kutoka visiwani Zanzibar, Feisal Salum Abdallah ‘Feitoto’ kwenda Azam FC, timu hiyo bado itaendelea kula fedha wakati nyota huyo atakapouzwa ndani au nje ya nchi.

Young Africans ilimuuza Fei Toto kwa Azam FC kwa dau lililofichwa kwa pande hizo mbili, lakini waliwekeana vipengele ambavyo timu hizo zitaendelea kunufaishana kwa mchezaji huyo.

Taarifa zinaeleza kuwa kwenye mkataba wa mauziano, Young Africans imeweka kipengele kwamba ikitokea Fei Toto anauzwa, basi klabu hiyo itapata sehemu ya fedha ya usajili.

Chanzo ndani ya Young Africans kinaeleza kuwa ikitokea Azam ikamuuza Feisal nje ya nchi, klabu hiyo itapata asilimia 25, hivyo kuwa biashara nzuri kwa mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Chanzo hicho kiliongeza kuwa Young Africans hawataki kuona mchezaji huyo akicheza tímu nyingine hapa nchini zaidi ya Azam FC, hivyo kuweka kipengele kigumu lakini chenye faida.

“Kwa hapa ndani tumeweka kwamba akienda katika timu yoyote ile, basi tunachukua Sh bilioni Moja, iwe kwa mkopo au kuuzwa,” kimesema chanzo hicho.

Habari zinaeleza kuwa Young Africans pia imelipwa Dola za kimarekani 120,000 ambazo ni takribani Sh 300 milioni kama ada ya uhamisho wa Fei Toto kwenda Azam FC.

Feisal amesaini mkataba wa miaka mitatu, ambao utamfanya akae kwenye timu hiyo Chamazi hadi 2026.

Samatta: Tutapambana ili tufuzu AFCON 2023
Jose Mourinho kutimkia Saudi Arabia