Uongozi wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Young Africans umekanusha taarifa zilizoanza kusambaa tangu juzi Jumatatu (Juni 26) majira ya jioni katika Mitandao ya Kijamii kuwa klabu hiyo imefungiwa kusajili kutokana na kushindwa kumlipa kocha wao wa zamani, Luc Eymael.
Taarifa hizo ziliwanyima raha baadhi ya Mashabiki na Wanachama wa Young Africans ambao waliamini huenda shughuli ya kushusha majembe ya uhakika katika kipindi hiki cha usajili.
Afisa Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ali Kamwe, amesema walikiri kupokea barua ya kumlipa kocha huyo tangu Machi 2023, na waliitolea ufafanuzi, huku kocha mwenyewe akithibitisha hilo, lakini anashangaa zilipotokea taarifa hizo.
“Hizi ni taarifa za uongo, hatujafungiwa na FIFA, hizi ni propaganda za watu walioshindwa, nawataka Wanachama na Mashabiki wa Young Africans kuzipuuza, wasiyumbishwe na maneno yasiyo ya kweli, taarifa kamili za klabu zitatolewa na vyombo vya klabu yenyewe,” amesema Kamwe.
Katika kusisitiza kuwa hazikuwa taarifa za ukweli, Kamwe amesema hazipo kwenye kurasa za Shirikisho la Kimataifa la Soka Duniani ‘FIFA’ hususan kwenye kitengo kinachoshughulikia suala hilo, ambapo kama zingekuwa sahihi zilitakiwa zianzie huko na kusambaa, siyo zionekane tu kwenye mitandao ya kijamii.
Hata hivyo, amekiri kuwa wanadaiwa na kocha huyo na walishaliweka suala hilo bayana, lakini kuhusu kumlipa, amesema si jambo la busara kuliweka hadharani.
“Tulikiri kupokea barua ya FIFA na makubaliano ilikuwa ni kumlipa kwa awamu, tukasema tunalifanyia kazi, ila siwezi kuja hadharani kueleza nini kinaendelea kwenye makubaliano haya ambayo yanafanyiwa kazi, haya ni mambo ya taasisi kwenda kwa mhusika mwenyewe, tunawaomba tu wanachama na mashabiki wa Young Africans kuwa watulivu.
“Tuko kwenye maandalizi ya msimu unaokuja, sasa hivi viongozi wanajiandaa kutoa jezi za msimu unaokuja, kutambulisha wachezaji wapya tunaowasajili kwa sababu hatujafungiwa na kuandaa ‘Pre Season’ kama unavyofahamu tutacheza mechi za Ngao ya Jamii mapema sana mwezi wa nane na safari hii zitachezwa kama ligi pamoja na Tamasha la Wiki ya Mwananchi,” Kamwe amezidi kufafanua.
Kocha huyo raia wa Ubelgiji aliifundisha Young Africans kuanzia Januari 2020 hadi Julai mwaka huo alipotimuliwa kwa madai ya kutoa maneno ya kibaguzi.
Tangu wakati huo kocha huyo amenukuliwa akidai anaidai klabu hiyo, ambapo Machi mwaka huu ziliibuka taarifa kama hizi za Young Africans kufungiwa madirisha matatu ya usajili, lakini mwenye Eymael aliibuka na kukiri anadai na kukanusha kuwa klabu hiyo imefungiwa.
“Nadhani walioandika taarifa hiyo wameripoti kinyume, tumejulishwa kwamba Young Africans wanatakiwa kunilipa stahiki zangu ndani ya siku 45 na iwapo wakishindwa kufanya hivyo kuna adhabu kubwa, ila hawajafungiwa kusajili, wamejulishwa uamuzi wa kutakiwa kunilipa fedha zangu,” amesema Eymael Machi mwaka huu.