Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Young Africans Dominick Albinus (Babaparoko), amekanusha taarifa za Kocha Mkuu wa klabu hiyo Nasrideen Nabi, kupewa michezo miwili kama mtihani wake wa mwisho klabuni hapo.
Mapema hii leo Jumanne (Septemba 14) baadhi ya vyombo vya habari na kwenye kurasa za mitandao ya kijamii, imedaiwa kuwa Kocha Nabi ametakiwa kushinda mchezo wa mkondo wa pili dhidi ya Rivers United ya Nigeria utakaochezwa ugenini mwishoni mwa juma hili, na kisha kuhakikisha anaifunga Simba SC kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii utakaochezwa Septemba 25, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Dominick Albinus (Babaparoko) amekanusha taarifa hizo kwa kuandika ujumbe kwenye Kundi (Group) la WhatsApp kwa kuandika:
MWANANCHI EPUKA PROPAGANDA
Leo kumezuka taarifa za uongozi wa Yanga kumpa kocha Mohammed Nabi mechi mbili zinazofuata kama hatima ya kibarua chake. Huu ni uzushi na uzandiki wa hali ya juu.
⚽ Uongozi una imani kubwa kwa kocha Nabi na una mipango naye ya muda mrefu sana kwa maendeleo na mipango ya muda mrefu katika kukifanya kikosi Cha Yanga kuwa tishio Afrika.
⚽ Hizi ni propaganda za maadui zetu na wasiotutakia mema. Niwahakikishie kuwa kocha Nabi yupo sana katika kikosi Cha wananchi.
⚽ Kocha Nabi ni miongoni mwa makocha wachache sana katika Afrika wenye elimu ya juu sana katika ufundishaji wa mpira wa miguu na hili linadhirishwa na mafanikio aliyoyapata alipokuwa anafundisha vilabu mbalimbali katika Afrika.
⚽ Huu ni wakati ambao wananchi wote tunapaswa kushikamana na kuonesha ukomavu wetu katika mpira wa miguu hapa nchini. Sisi ni wananchi na daima hatujawahi kukata tamaa.
⚽ Kikosi kiko katika mikono salama ya makocha wetu, viongozi pamoja na wadhamini wetu na kamwe haturudi nyuma.
⚽ Epuka matapeli Nabi yupo sana na kinachofanywa ni kuogopa kivuli chake katika ligi kuu Tanzania kwani nusu ya msimu uliopita walikiona Cha moto nna hofu imewatanda.”