Uongozi wa Young Africans umesitiza juu ya kumalizana na wachezaji wote ambao walikuwa wakiwahitaji, huku wakiweka wazi kuwa hakuna mchezaji mwingine yeyote ambaye walikuwa wanamhitaji ambaye hawajamalizana naye.
Young Africans mpaka sasa wamemtambulisha mchezaji mmoja, mzawa winga Nickson Kibabage kutoka Singida Fountain Gate alikokuwa kwa mkopo akitokea Mtibwa Sugar huku kwa wachezaji wa kigeni wakiwa bado hawajaanza kazi.
Young Africans wanahusishwa kukamilisha usajili wa wachezaji wengine kama Maxi Mpiana kutoka DR Congo, Aubin Kramo kutoka Ivory Coast, Jonas Mkude aliyeachwa Simba SC na Mohamed Zougrama kutoka Asec Mimosas.
Makamu wa Rais wa Young Africans, Arafat Haji amesema kuwa wao kama uongozi tayari walishakamilisha usajili wa wachezaji wote ambao walikuwa wakiwahitaji hivyo hakuna mchezaji mwingine ambaye wanamfukuzia kwa sasa.
“Young Africans tayari tumekwishamaliza taratibu zote za kuwasajili wale wachezaji wote ambao tulitaka kuwasajili kwa msimu huu hivyo hakuna mchezaji mwingine yeyote ambaye tunamhitaji na tunamfuatilia.
“Kwa sasa ambacho tunakifanya ni kuhakikisha kuwa tunafuata taratibu zetu za utambulisho kupitia kitengo chetu cha habari na mawasiliano, kwani ndio jambo ambalo linafuata muongozo wa kiofisi na makubaliano ya ukuaji katika sekta hiyo ya habari ya Young Africans,” amesema kiongozi huyo.