Uongozi wa klabu ya Young Africans umesema umepanga kikosi chao kishiriki michuano ya kimataifa msimu ujao kwa nguvu zao wenyewe na wala si kwa kubebwa na timu yoyote, kutoka nchini.

Afisa Habari wa Young Africans, Hasan Bumbuli amesema nia yao msimu huu ni kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ili kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa tiketi yao wenyewe na si ya kukatiwa na timu nyingine.

Bumbuli amesema hayo alipoulizwa juu ya ushindi wa Simba SC wa mabao 4-1 dhidi ya AS Vita ambao umeiweka Tanzania kwenye mazingira mazuri ya kuongeza timu 4 msimu ujao kwenye michuano ya kimataifa.

“Mimi sijasikia matokeo yoyote ya Simba SC, ila kama wameshinda basi sawa, lakini kusema eti watatubeba kwenye michezo ya kimataifa, labda wawabebe wengine siyo sisi.

“Young Africans tutakwenda kwa nguvu zetu wenyewe kwenye michuano ya kimataifa kwa sababu kwa sasa tunaongoza ligi na tunausaka ubingwa, nina imani tutaupata na hatutohitaji kutafutiwa nafasi na mtu,” amesema Bumbuli.

Young Africans kwa sasa inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kufikisha alama 50 baada ya michezo michezo 23 waliocheza, ikifuatiwa na mabingwa watetezi Simba SC wenye alama 46 zilizopatikana kwenye michezo 20 waliyocheza mpaka sasa.

Kanuni wa TFF zinaeleza kuwa, timu bingwa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara itashiriki Michuano ya Klabu Bingwa Barani Afrika na bingwa wa Kombe la Shirikisho (ASFC) atashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Korea Kaskazini: Kwetu hakuna Corona
SADC yaitisha Mkutano wa dharura, Rais Mwinyi amwakilisha Rais Samia