Klabu ya Young Africans imekanusha uvumi wa kumuwani Mshambuliaji kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati na klabu ya Vipers ya Uganda Cesar Manzoki.
Young Africans imetajwa mara kadhaa katika kipindi hiki cha kuelekea mwishoni mwa msimu huu, huku ikihusishwa kumsaka Mshambuliaji ambaye atasaidiana na Fiston Mayele msimu ujao wa Ligi Kuu na jina la Manzoki limekuwa likitajwa.
Mjumbe wa Kamati ya Usajili ya Young Africans Hersi Said amesema taarifa za klabu hiyo kuhusishwa na mpango wa kumuwania Mshambuliaji huyo sio za kweli, na hawakuwahi kujihusishwa na mpango huo.
Amesema taarifa za usajili wa Manzoki wamekua wakiziona katika mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari, lakini ukweli ni kwamba Young Africans haikujihusishwa na mpango wa kuhitaji kumsajili.
“Hapana, hatujawahi kumhitaji Cesar Manzoki, na hizi taarifa zimekua zikisemwa kwenye mitandao ya kijamii na hata kwenye magazeti, lakini ukweli ni kwamba hatujawahi hata kuwasiliana naye”
“Huenda ni mchezaji mzuri na ndio maana anahusishwa na Young Africans, lakini sisi tuna mpango wetu wa usajili na hautakuwa wazi kama unavyozungumzwa huko nje, Mashabiki na Wanachama waendelee kuwa watulivu timu yao itasajili na watafahamishwa kwa njia sahihi, sio mitandao ya kijamii.” amesema Hersi Said.
Cesar Manzoki ambaye ni mzaliwa na DR Congo amemaliza mkataba na klabu ya Vipers huku klabu kadhaa zikitajwa kumuwania katika kipindi hiki cha kuelekea msimu mpya wa 2022/23.