Kinda Kutoka nchini Uganda Allan Okello amekiri kuvutiwa na Klabu ya Young Africans inayoendelea kufanya vizuri katika Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu wa pili mfululizo.
Young Africans inashikilia Taji la Ligi Kuu ikiwa inaendeleza Rekodi ya kucheza michezo 48 bila kufungwa tangu msimu wa 2020/21, ambapo kwa mara ya mwisho ilipoteza dhidi ya Azam FC kwa bao 1-0.
Okello anayecheza kwa mkopo KCCA ya nchini kwao Uganda akitokea Paradou AC ya nchini Agleria amesema, ikitokea Uongozi wa Young Africans unaonyesha nia ya kumsajili, atakuwa tayari kujiunga na klabu hiyo ya Tanzania.
Amesema anaifuatilia kwa ukaribu Young Africans na anapendezwa na uchezaji wake inapokua katika harakati za Kusaka alama tatu muhimu katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara, hivyo ikitokea anatakiwa klabuni hapo hatokataa katu.
“Ninaipenda Young Africans, nimekua ninaifuatilia kila siku inapocheza, kwa kweli ninafurahia namna wanavyocheza na kuendelea kupata matokeo mazuri,”
“Hakuna ubishi kwa sasa Young Africans ina kikosi Bora katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, hali ambayo inawafanya Wachezaji wengi kutamani kujiunga na Klabu hiyo ya Jangwani-Dar es salaam.” amesema Okello
Hata hivyo Kinda hilo ambalo liliwahi kutamba na Kikosi cha vijana chini ya Umri wa miaka 17, limesisitiza kuheshimu misingi na makubaliano ya kimkataba yaliopo kati yake na Klabu ya Paradou AC, hivyo ametoa angalizo kwa yoyote anayehitaji huduma yake anapaswa kuzungumza na Uongozi wa Klabu hiyo.