Uongozi wa Young Africans umefunguka na kusawazisha taarifa zinazomuhusu Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ghana Bernard Morrison ambaye anadaiwa kutaka kuihujumu timu hiyo ilipokuwa nchini Nigeria kwa ajili ya mchezo wa Robo Fainali, Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Morrison licha ya kusafiri na timu kwenda Nigeria kwa ajili ya mchezo kati ya Young Africans dhidi ya Rivers hakuwepo katika sehemu ya kikosi kilichoshiriki mchezo huo na kuzua sintofahamu nyingi kwa mashabiki wao.
Jumapili (April 23), Young Africans ilikuwa ugenini Nigeria kucheza mchezo wa mkondo wa kwanza wa Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya wenyeji wao Rivers na kushinda mabao 2-0.
Afisa Habari wa Young Africans, Ally Kamwe amesema kuwa wao wenyewe walishitushwa na taarifa za Morrison kutaka kuwahujumu huku wakiweka wazi kuwa taarifa hizo ni za uzushi kwani hazina ukweli wowote na anaamini watu waliofanya hivyo walikuwa wanafanya kwa lengo la kuwatoa mchezoni.
“Tulishangazwa sana na taarifa za watu juu ya mchezaji wetu Bernard Morrison kutaka kutuhujumu, hawa watu bila shaka walitaka kututoa mchezoni kuelekea katika mchezo wetu dhidi ya Rivers, bahati mbaya kwao Young Africans hii sio timu wanayoifahamu wao.
“Morrison kama kweli alikuwa na mpango wa kutuhujumu sisi tusingempeleka katika mahojiano na Waandishi wa Habari kuelekea katika mchezo wetu, na kwa faida tu ya watu Morrison aliumia kabla ya mchezo na ndio maana hakucheza, alipata majeraha ya goti na hicho ndio chanzo cha yeye kukaa nje na kuwapisha wengine kucheza,” amesema kiongozi huyo