Huku wakijiandaa na vita kali ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya timu za Waarabu, Al Ahly, CR Belouzdad na Medeama ya Ghana Benchi la Ufundi la Young Africans limewasilisha ripoti fupi kwenda kwa uongozi wa timu hiyo, juu ya kutaka mshambuliaji mpya ambaye ametimia kweli kweli.
Safu ya ushambuliaji ya Young Africans kwa sasa inaongozwa na Washambuliaji wanne ambao ni Clement Mzize, Kennedy Musonda, Hafiz Konkoni na Chrisprin Ngushi, lakini bado benchi la ufundi halijatosheka na huduma za baadhi ya washambuliaji hao ambapo imefahamika kuwa miongoni mwa mastaa wanaotajwa kuwindwa na Young Africans ni, Andy Boyeli wa Power Dynamos.
Kati ya washambuliaji hao waliopo ni Clement Mzize na Kennedy Musonda pekee ndio huwa wanapata nafasi ya kucheza kwa kupishana mara kwa mara huku ingizo jipya, Hafiz Konkoni ambaye ni ingizo jipya pamoja na Ngushi wakiwa hawapati nafasi ya mara kwa mara ya kucheza.
Chanzo cha ndani ya Young Africans kimeeleza juu ya benchi hilo la ufundi kupelekea ripoti ndogo kwa viongozi wa Young Africans baada ya kumalizika kwa mechi 5 za ligi na timu kutinga makundi ya Ligi ya Mabingwa huku ripoti hiyo ikionyesha mahitaji katika eneo la ushambuliaji kuhitaji ingizo jipya pale ambapo dirisha la usajili litafunguliwa.
“Ni kweli benchi la ufundi limepeleka ripoti ndogo ambayo wameiandaa chini ya kocha mkuu na wasaidizi wake, ripoti hiyo imezungumzia maendeleo ya timu lakini wameonyesha ni kwa jinsi gani kuna uhitaji wa usajili katika eneo la ushambuliaji.
“Benchi la ufundi limeona kuna ulazima wa kuwaongezea nguvu washambuliaji waliopo kwenda kushindana katika hatua ya makundi na mashindano mengine wanayoshiriki.”
Hivi karibuni Kocha Mkuu wa Young Africans, Miguel Gamondi alisema: “Ili Young Africans tuweze kwenda kushindana vizuri katika Ligi ya Mabingwa Barani Afrika tunahitaji kufanya usajili kwa ajili ya kuongezea nguvu kikosi chetu, tunakwenda katika hatua ngumu lazima tuongeze ubora wetu ili tukashindane na wala sio kwenda kushiriki,” amesema Gamondi.