Kikosi cha Young Africans kimeanza safari ya kurejea jijini Dar es salaam, kikitokea mkoani Kagera kilipokua na shughuli ya mchezo wa mzunguuko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar jana Jumatano (Septamba 29), katika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Katika mchezo huo Young Africans ilichomoza na ushindi wa bao 1-0, lililopachikwa wavuni n a kiungo kutoka visiwani Zanzibar Feisal Salim ‘Fei Toto’ na kuifanya klabu hiyo yenye maskani yake katika makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani jijini Dar es salaam, kuanza vyema msimu mpya wa 2021/22.

Kurasa za mitandao ya kijamii za klabu hiyo zimethibitisha kuondoka kwa kikosi chao, kwa kuweka picha zikiwaonesha wachezaji na viongozi wa benchi la ufundi wakipanda ndege ya shirika la ndege la Tanzania (Air Tanzania), katika Uwanja wa ndege wa Bukoba, mkoani Kagera.

Young Africans itacheza mchezo wa mzunguuko wa pili Jumapili (Oktoba 03) dhidi ya Geita Gold FC katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Geita inayoshiriki kwa mara ya kwanza Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara ilianza vibaya msimu huu kwa kufungwa mabao 2-0 dhidi ya Namungo FC, ikiwa ugenini mkoani Lindi.

Serikali kuja na mikakati ya ulipaji kodi na misamaha
Azam FC: Tunautaka ubingwa 2021/22