Hatimaye Klabu Bingwa Tanzania Bara Young Africans imefanya usajili wa Kimataifa kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ mapema leo Ijumaa (Julai 21).
Taarifa iliyotolewa mapema jana Alhamis (Julai 20) na TFF, ilionesha Young Africans ilikuwa haijasajili mchezaji yoyote upande wa Kimataifa, hali ambayo ilizua taharuki kwa wadau wengi wa Soka nchini Tanzania.
Hata hivyo hadi sasa Klabu hiyo inayoshikilia Taji la Tanzania Bara kwa msimu miwili mfululizo, imefanya usajili wa wachezaji 21, huku idadi ya usajili kwa klabu za Simba SC ikiongezeka, Azam FC ikisalia wachezaji Saba na Singida Fountain Gate akipungua mchezaji mmoja, kwa mujibu wa taarifa ya leo Ijumaa.
Taarifa ya jana Alhamis ilionesha Simba SC ilikuwa imefanya usajili wa Wachezaji 24, lakini leo Ijumaa inaonesha imeshasajili Wachezjai 26, huku Singida Fountain Gate idadi ikipunguwa kutoka 23 hadi 22.
Ikumbukwe kuwa Young Africans na Simba SC zitaiwakilisha Tanzania katika Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika huku Singida Fountain Gate na Azam FC zikijipanga kushiriki Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu ujao 2023/24.