Mwandishi wa Habari za Michezo Gift Macha amesema, Kikosi cha Young Africans kimeimarika kwa kiasi kikubwa, baada ya kuambulia alama moja kwenye Mchezo wa Mzunguuko watatu, Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Jana Jumapili (Februari 26) Young Africans ilicheza ugenini mjini Bamako-Mali dhidi ya AS Real Bamako katika Uwanja wa Machi 26, na kuambulia sare ya 1-1.
Gift Macha ambaye pia ni Mtozi wa vipindi vya Michezo Azam TV (Azam Media), amesema kikosi cha Young Africans kimekua na muonekano tofauti na ilivyokuwa msimu ulipopita, hivyo anaamini kinaweza kufanya makubwa na maajabu kwenye Michuano ya Kimataifa msimu huu.
Amesema katika mchezo wa Jana Jumapili, Young Africans ilicheza bila kuogopa ugenini, na kikosi chake kilikuwa chepesi kukaba kilipopoteza mpira, huku kikimiliki vizuri dhidi ya wapinzani wao.
“Young Africans wameimarika sana kama timu. Wanamiliki mpira vizuri.. Wakipoteza wanakaba kwa haraka sana. Wana kasi katika kushambulia na pia wana wachezaji mahiri wa kuamua mechi. Nazidi kuwaona mbali.” amesema Gift Macha
Katika mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi kutoka nchini Botswana Joshua Bando, Young Africans ilitangulia kupata bao kupitia kwa Mshambuliaji kutoka DR Congo Fiston Kalala Mayele dakika ya 60 kabla ya Kone hajafunga bao la kusawazisha dakika ya 90.
Young Africans itaendelea na Mbilinge Mbilinge za Kombe la Shirikisho Barani Afrika Jumatano (Machi 08) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, kwa kuikaribisha AS Real Bamako.