Kuelekea mchezo wao wa Fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania bara ‘ASFC’ dhidi ya Azam FC utakaopigwa keshokutwa Jumatatu (Juni 12), uongozi wa Young Africans umetamba kuwa tayari umemaliza maandalizi yote kuelekea mchezo huo na kuchimba mkwara mzito kuwa ubingwa ni lazima.
Young Africans wanaelekea katika mchezo huo wa keshokutwa, wakiwa mabingwa wa Tanzania Bara kwa mara ya pili mfululizo, na leo Jumamosi wanalitembeza Kombe la ubingwa katika baadhi ya mitaa ya jiji la Dar es salaam.
Mbali na Ubingwa wa Tanzania Bara, Young Africans pia wataingia katika mchezo huo wa Fainali wakiwa na kumbukumbu nzuri ya kushinda ubingwa wa ASFC msimu wa 2021/22 mara baada ya kuibuka na ushindi wa mikwaju ya Penati dhidi ya Coastal Union mchezo uliopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Afisa Habari wa Young Africans Ally Kamwe amesema: “Mara baada ya kufunga hesabu zetu za Ligi Kuu kwa msimu huu jana baada ya mchezo wetu dhidi ya Prisons kikosi chetu kitarejea Dar es salaam kwa ajili ya sherehe za ubingwa kabla ya kuanza safari ya kwenda Tanga.
“Maandalizi yote ya mchezo wa fainali yamekamilika na sasa kilichobaki ni wachezaji wetu kumaliza kazi uwanjani, tumedhamiria na tunaamini ni lazima kwetu kutetea kombe letu.”