Uongozi wa mabingwa wa soka Tanzania Bara, Young Africans umesema kikosi chao kimeelekea jijini Tanga kwa lengo moja tu, kutetea ubingwa wa Ngao ya Jamii waliotwaa msimu uliopita.

Young Africans wanashikilia ubingwa huo kwa misimu miwili mfululizo na mara zote wamefanya hivyo kwa kuwafunga wapinzani wao wakubwa Simba SC.

Msimu wa mwaka 2021/22 Young Africans waliwafunga Simba SC bao 1-0 Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa bao la Fiston Mayele na msimu wa mwaka 2022/23 waliifunga tena Simba SC mabao 2-1 na yote yakifungwa na Mayele ambaye hatakuwa sehemu ya timu hiyo kwa msimu ujao kwani ameuzwa kwenye klabu ya Pyramid ya Misri.

Afisa Habari wa klabu hiyo, Ali Kamwe amesema wanaenda Tanga ambapo mashindano ya Ngao ya Jamii yanafanyika kwa lengo moja tu la kutetea taji hilo ambapo kesho Jumatano (Agosti 09) watafungua dimba kwa kucheza na Azam FC, katika Uwanja wa Mkwakwani.

“Kama uongozi tumedhamiria kushinda mataji yetu yote tuliyotwaa msimu uliopita na tunaanza na hili la Ngao ya Jamii. Tuna kikosi kizuri, Benchi bora la Ufundi na tumefanya maandalizi mazuri mpaka sasa. Tunaamini tutatimiza dhamira yetu.” amesema Kamwe

Amesema Rais wa klabu hiyo, Hersi Said amekuwa mstari wa mbele kuwahamasisha na kuwaeleza wachezaji umuhimu wa kutetea taji hilo na kilichobaki upande wa wachezaji na Benchi la Ufundi ni kutekeleza dhamira hiyo.

Kamwe amesema wachezaji wote kwenye kikosi cha timu hiyo wako katika hali nzuri na hakuna hata mmoja aliye na majeraha.

Kikosi cha wachezaji 27 na Benchi la Ufundi la klabu ya Young Africans kiliondoka jijini Dar es salaam jana Jumatatu (Agosti 07) kuelekea Tanga kwa ajili ya michuano hiyo ambapo kesho Jumatano (Agosti 09) kitafungua dimba dhidi ya Azam FC katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Mikel Arteta afichua siri ya Penati
Muhogo kuwapa tabasamu Watanzania 600