Kikosi cha klabu ya Young Africans mapema hii leo kiliwasili mjini Dodoma kikitokea Dar es salaam, tayari kwa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaowakutanisha dhidi ya maafande wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT Tanzania).

Young Africans watakuwa wageni wa maafande hao kesho Jumatano (Mei 19)  kwenye uwanja wa Jamhuri, mjini Dodoma kuanzia mishale ya saa kumi jioni.

Baada ya kuwasili Uwanja wa ndege wa Dodoma, kikosi cha Young Africans pamoja na benchi lao la ufundi kilikwenda moja kwa moja bungeni, kufuatia mwaliko wa wabunge ambao ni mashabiki wa klabu hiyo kongwe nchini Tanzania.

Young Africans leo jioni watafanya mazoezi kwenye uwanja wa Jamhuri, ili kukamilisha program ya mazoezi ya Kocha Nabi, ambaye tangua lipoanza kazi yake klabuni hapo ameambulia alama moja pekee katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara, kwa kupata matokeo ya sare ya bila kufungana dhidi ya Namungo FC.

Kocha huyo kutoka nchini Tunisia, alianza kazi rasmi Young Africans katika mchezo dhidi ya Azam FC ambao ulishuhudia wananchi wakilambishwa shubiri kwa kufungwa bao moja kwa sifuri, na baada ya hapo aliibuka na ushindi wa bao moja kwa sifuri dhidi ya Tanzania Prisons kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho (ASFC).

 Young Africans inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kufikisha alama 58, wakitanguliwa na Simba SC wenye alama 61, huku Azam FC wakishika nafasi ya tatu kwa kufikisha alama 57.

Wachezaji KMC FC wapewa mapumziko
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Mei 18, 2021