Kikosi cha Young Africans, leo Al-Khamis Septemba 17 kimewasili mjini Bukoba mkoani Kagera kwa ajili ya mchezo wa mzunguuko watatu wa Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar kikiwa kimebeba matumaini kibao ya kuibuka na ushindi.

Kikosi cha mabingwa hao wa kihistoria katika soka la Bongo kilianza safari mapama leo asubuhi jijini Dar es salaam na kuchukua muda wa saa moja na dakika kadhaa kuwasili uwanja wa ndege mjini Bukoba mkoani Kagera.

Young Africans wamesafiri huku wakiwa na chagizo la la ushindi wa mabao mawili kwa sifuri uliopatikana jana, Septemba 16 Uwanja wa Azam Complex dhidi ya Mlandege FC kwenye mchezo wa kirafiki.

Mchezo huo ambao ulikuwa na malengo ya kuboresha kikosi hicho ambacho hakijawa na muda mrefu wa kufanya mazoezi kwa pamoja ulikuwa ni wa ushindani mkubwa kwa timu zote mbili.

Mabao ya Young Africans yalipachikwa kimiani na nyota wake wapya ambao ni pamoja na Wazir Junior aliyesajiliwa kutoka Mbao FC pamoja na Tunombe Mukoko aliyetua klabuni hapo akitokea AS Vita ya DR Congo.

Young Africans itamenyana na Kagera Sugar, Septemba 19 Uwanja wa Kaitaba ambapo inashuka uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kushinda bao moja kwa sifuri kwenye mchezo wa ligi mbele ya Mbeya City.

Kagera Sugar wao walitoka kulazimisha sare ya bila kufungana mbele ya Gwambina FC. Unakuwa ni mchezo wa pili kwa Kagera Sugar kucheza wakiwa nyumbani ambapo ule wa kwanza walipoteza kwa kufungwa bao moja kwa sifuri dhidi ya JKT Tanzania.

Kwa upande wa Young Africans ni mchezo wa kwanza kucheza nje ya Dar es salaam msimu huu 2020/21, ambapo mchezo wa kwanza dhidi ya Tanzania Prisons waliambulia sare ya kufungana bao moja wa moja pamoja na ushindi wa bao moja kwa sifuri dhidi ya Mbeya City yote ikichezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Zaidi ya wafungwa 200 watoroka
Msaidizi wa Membe yuko salama - SACP Mambosasa

Comments

comments