Kikosi cha Young Africans kimewasili salama mjini Ruangwa Mkoani Lindi tayari kwa mchezo wa Mzunguuko wa 15 wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Namungo FC.
Mpambano huo wa kukamilisha Duru la Kwanza msimu huu 2022/23 umepangwa kuchezwa kesho katika Uwanja wa Majaliwa mjini Ruangwa, huku wenyeji Namungo FC wakijipanga kuibomoa Young Africans yenye dhamira ya kuendelea kukaa kileleni mwa msimamo.
Young Africans imewasili Ruangwa ikitokea mkoani Mtwara, ambako kilishuka na Ndege jana Jumatatu (Desemba 05) ikitokea jijini Dar es salaam.
Baadhi ya Mashabiki na Wanachama wa Young Africans wameonesha mapenzi kwa Wachezaji na Viongozi walioambatana na kikosi mjini Ruangwa kwa kuwapokea kwa shangwe kubwa.
Young Africans hadi sasa inaongoza Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 35 sawa na Azam FC, huku Simba SC ikishika nafasi ya tatu kwa kufikisha alama 34.
Namungo FC ipo nafasi ya tisa ikiwa na alama 18, ikishinda michezo mitano, ikitoka sare mitatu na kupoteza sita.