Uongozi wa Young Africans una matumaini makubwa ya kikosi chao kucheza Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu huu 2022/23, baada ya kuonesha uthubutu wa kupambana na miamba mikubwa Barani humo.
Young Africans ipo hatua ya Robo Fainali ikiwa na faida ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Rivers United ya Nigeria, huku ikitarajia kucheza mchezo wa Mkondo wa Pili wa Robo Fainali mwishoni mwa juma hili katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Afisa Habari wa Klabu hiyo Kongwe katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati Ally Shaban Kamwe amesema, hakuna timu ya kuwazuia kubeba ubingwa wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu huu, kwani wana kikosi bora na Benchi zuri la Ufundi chini ya Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi.
“Zamani Young Africans haikuwa kwenye nafasi nzuri katika mashindano ya kimataifa, lakini sasa imethubutu, hatua ya makundi tumemaliza nafasi ya kwanza.”
“Baada ya hapo tukaingia Robo Fainali, tumeshinda mchezo wetu wa kwanza ugenini, tuna faida ya mabao mawili na mchezo ujao tutakuwa nyumbani.”
“Njia ya Nusu Fainali tunaiona ni nyeupe, ukivuka huko chochote kinaweza kutokea, kwa nini isiwe; Young Africans ikapata nafasi ya kuchukua ubingwa huu wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika? Itakuwa furaha kwa mashabiki, viongozi na Tanzania kwa ujumla. Naona Young Africans wakiwa mabingwa kabisa.”