Young Killer Msodoki ameweka wazi sababu za kuamua kuachana na menejimenti ya Wanene Entertainment, baada ya kukamilisha miezi sita ya mkataba wake.
Killer amesema kuwa alichokuwa anatarajia kukipata ndani ya kampuni hiyo hakufanikiwa kukipata na kwamba badala yake aliona ni bora alipokuwa anafanya kazi akiwa mwenyewe.
Akifunguka wiki hii kupitia The Playlist ya Times FM, Young Killer amesema kuwa moja kati ya mambo aliyokuwa anayatarajia lakini hakuyaoni ni pamoja na kukuza wigo wa muziki wake nje ya mipaka ya Tanzania.
“Unajua hakuna kitu kizuri katika muziki wetu kama mafanikio ya kuzidi kupata connection tofauti-tofauti. Pia, nilikuwa nategemea kuona nyimbo zangu hata zinapigwa ‘Trace’, ili kuleta utofauti wa Young Killer yule ambaye alikuwa anafanya kazi mwenyewe na huyu ambaye anafanya kazi na Menejimenti kubwa kama Wanene. Hiyo ni moja ya mambo, lakini vitu ni vingi,” Killer amefunguka.
Mkali huyo wa ‘Secreto’ alifunguka zaidi kuwa baada ya kuona mambo hayaendi vizuri, aliamua kuwasilisha barua yake mapema kwa uongozi wa Wanene kuhusu nia yake ya kutoongeza muda wa mkataba wao, na ilipofika muda waliachana kwa mujibu wa mkataba.
Rapa huyo amesema kuwa yuko tayari kufanya kazi na Lebo nyingine za muziki endapo ataridhika kuwa zitampigisha hatua.
Young Killer alifanya kazi bila Menejimenti kwa takribani mine mfululizo, baada ya kuachana na meneja wake wa kwanza ambaye alikuwa mpishi wa ngoma zake, Mona Gangster wa Classic Sound.
Alitangaza kujiunga na Wanene April 13 mwaka huu na kuachia ngoma kadhaa ikiwa ni pamoja na ‘Hunijui’, akiwashirikisha Dully Sykes na Ben Pol. Nyingine ni Shots akiwa na Khaligraph Jones wa Kenya.