Klabu ya Aston Villa imekubali dili la kumsajili mchezaji wa kimataifa wa Ubelgiji, Youri Tielemans kutoka Leicester City iliyoshuka daraja.
Villa imethibitisha kuwa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 26 atajiunga nao Julai 1 baada ya miaka minne katika uwanja wa King Power.
Taarifa kwenye tovuti rasmi ya klabu ilisema: “Aston Villa ina furaha kutangaza kwamba klabu imefikia makubaliano ya kumsajili Youri Tielemans.
“Mchezaji wa kimataifa wa Ubelgiji, Youri Tielemans atakuwa Villan rasmi Julai 1 baada ya mkataba wake na Leicester City kumalizika.”
Youri Tielemans
Tielemans alijiunga na Leicester kutoka Monaco kwa mkataba wa pauni milioni 40 mnamo Julai 2019 baada ya kufanikiwa kwa mkopo katika kipindi cha pili cha msimu uliopita, baada ya kuanza kazi yake na Anderlecht.
Kwa jumla, aliichezea mechi 195 na kufunga mabao 28, likiwamo bao la ushindi walipoichapa Chelsea 1-0 kwenye fainali ya Kombe la FA 2021.
Pia aliwakilisha nchi yake kwenye fainali za Kombe la Dunia za 2018 na 2022 na Euro 2020.