Shirikisho la soka nchini Tunisia lina imani kubwa ya kumuona mshambuliaji Youssef Msakni, kwenye kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo kitakachoshiriki fainali za kombe la dunia mwezi Juni nchini Urusi.
Msakni, amezusha hofu ya kutokuwa sehemu ya kikosi cha Tunisia kitakachoshiriki fainali hizo, kufutia majeraha ya goti aliyoyapata mwishoni mwa juma lililopita, alipokua katika jukumu la kuitumikia klabu yake ya Al Duhail katika ligi ya nchini Qatar.
Mshambuliaji huyo ambaye alikua mwiba wakati wa michezo ya kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia kanda ya Afrika, alithibitisha kutokua na uhakika wa kucheza fainali hizo, kupitia kurasa za mitandao ya kijamii.
Hata hivyo uongozi wa klabu ya Al Duhail umeanza jitihada za kumtibu Msakni, na tayari umeshaeleza mikakati ya kumsafirisha kwenda nchini Marekani kwa ajili ya kufanyiwa matibabu ya hali ya juu.
Kwa upande wa shirikisho la soka nchini Tunisia limemuagiza daktari wa kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo Souheil Chemli, kuhakikisha anafuatilia kwa ukaribu maendeleo ya Msakni, na ikwezekana kuwa naye karibu katika kipindi chote atakachokuwepo Marekani kwa matibabu.
Tunisia wamepangwa katika kundi G, na wataanza kampeni za kusaka ubingwa wa dunia kwa kucheza dhidi ya England mjini Volgograd Juni 18, kisha watapapatuana na Ubelgiji mjini Juni 23 na kumalizia na Panama katika mji wa Saransk siku tano baadae.