Kocha Mkuu wa Azam FC, Youssouph Dabo amewaambia wachezaji wake kuonesha thamani yao ya juu katika kila mchezo ukiwemo wa dhidi ya Young Africans utakaopigwa Jumatatu, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.

Dabo amesema anawafahamu Young Africans kwa kuwa alikutana nao kwenye mechi ya Ngao ya Jamii na kufungwa mabao 2-0 lakini anaamini hii ni mechi nyingine na amewaandaa wachezaji wake kwa namna nyingine.

“Nimewaeleza wachezaji wangu tangu tumeanza msimu kwamba hatuchezi na mpinzani mmoja au wawili, tunapaswa kucheza vizuri kila wakati, kupambana na kuonesha thamani yetu kwa kushikamana na utayari kila mchezo, hilo ndio la muhimu.

“Na sasa tunakutana na Young Africans, timu ambayo tulikutana nayo Tanga (Uwanja wa Mkwakwani) katika Ngao ya Jamii, ulikuwa wakati mzuri kuwafahamu lakini huu ni mchezo mwingine na kuna utofauti tangu wakati ule na sasa hivyo tunaendelea kujiandaa tukitazamia kukua zaidi kila wakati,” amesema Dabo raia wa Senegal.

Timu hizo zinakutana wakati Azam ikiwa juu kwenye nafasi ya pili kwa pointi 13 baada ya ushindi wa medhi nne na sare moja, huku Young Africans ikiwa nafasi ya tatu kwa pointi 12 ilizovuna baada ya ushindi wa mechi nne na kufungwa mchezo mmoja.

Mahakama yapigilia msumari ununuzi Kampuni ya Saruji
Katwila atanguliza mguu moja Mtibwa Sugar