Mtandao wa kuweka video wa YouTube umepiga marufuku video za mashindano yanayoweza kuhatarisha maisha ya binadamu.
Mtandao huo unaomilikiwa na kampuni ya Google, umeeleza kuwa inaanza kuifanyia kazi sera yake ya kutopokea video zenye kuhatarisha maisha ya binadamu, baada ya kuona kuwa zinawekwa kwa wingi na kuangaliwa na mamilioni na walioziweka wakijipatia fedha nyingi.
“YouTube ni nyumbani kwa video nyingi za mashindano zinazozua gumzo. Na tumekuwa na sera ambazo zinahakikisha kuwa vitu vinavyofurahisha havivuki mipaka na kuwa hatari kwa maisha,” imeeleza taarifa ya YouTube.
“Miongozo yetu inakataza video ambazo zinahamasisha matendo ya hatari au zinazoweza kusababisha hatari, na leo tunafafanua kwa kuzingatia video zilizoongezeka za mashindano ya hatari pamoja na kushtuana kunakoweza kuleta hatari (dangerous prank),” imeongeza.
Imefafanua kuwa hatua hiyo itahusu pia video zinazoweka mitego ya kumuonesha mtu kuwa yuko kwenye hatari kubwa wakati ambapo hayuko kwenye hatari, kwa lengo la kumuogofya.
YouTube wameongeza kuwa video yeyote ambayo inaonekana kuwa inaweza kudhuru saikolojia ya mtoto baada ya kuitazama, itashushwa mara moja na aliyeiweka atapigwa marufuku.