Imefahamika kuwa Klabu ya Geita Gold imenasa saini ya aliyekuwa wa Mshambuliaji wa Kagera Sugar, Yusufu Mhilu na kumpatia mkataba wa mwaka mmoja.

Nyota huyo wa zamani wa Simba SC amejiunga na kikosi hicho baada ya mkataba wake na Kagera Sugar aliyokuwa anaitumikia kwa mkopo kufikia kikomo mwishoni mwa msimu uliopita 2022/23.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Geita, Simon Shija amesema hadi sasa tayari wamekamilisha baadhi ya sajili mpya.

“Ni kweli tumefanya maboresho ya kikosi chetu kama ilivyokuwa utaratibu kwenye kila msimu, ila sitaki kuweka wazi sana hadi tutakapofikia makubaliano kwa sababu kuna wachezaji tunaweza kuwataja mwishowe wakaondoka kabla dili halijatimia,” amesema.

Hata hivyo, licha ya Shija kutoweka wazi, imefahamika kuwa nyota huyo aliyefunga bao moja tu kwenye Ligi Kuu msimu uliopita ataungana na kikosi hicho baadae leo Jumamosi (Julai 22), ili kuanza maandalizi rasmi ya msimu mpya ‘Pre Season’.

Usajili huo ni wa tatu kukamilika kwa Geita baada ya kipa Erick Johola aliyetokea Young Africans na Tariq Simba wa Polisi Tanzania.

Geita imeachana na Danny Lyanga, George Wawa, Deus Okoyo, Shinobu Sakai, Arakaza MacArthur, Shown Oduro, Jeremiah Thomas, Jofrey Manyasi na Juma Liuzio.

Mlinda Lango wa Cameroon akamilisha Simba SC
Wahalifu 106 watupwa Gerezani Arusha