Kiungo wa Singida Fountain Gate, Yusuph Kagoma amesema anaamini Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao 2023/24, itakuwa ngumu kutokana na namna kila timu inavyosajili kwa sasa.
Kagoma ambaye alijiunga na timu hiyo Dirisha Dogo msimu uliopita akitokea Geita Gold FC na alikuwa sehemu ya Wachezaji walioiwezesha Singida kumaliza katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Akizungumza akiwa jijini Arusha timu hiyo ilipoweka kambi kujiandaa na msimu mpya wa ligi ambayo itaanza Agosti 15, mwaka huu, Kagoma amesema anaamini msimu ujao utakuwa ngumu kwani kila timu imesajili vyema.
Amesema kama mchezaji mikakati yake ni kuendelea kupambana kwa kushirikiana na wenzake ili kuhakikisha ligi ikianza na mashindano ya kimataifa waiwezeshe timu kumaliza kwenye malengo ambayo yatakuwa yamewekwa hivyo anaamini kambi ya Arusha itawabeba.
“Msimu ujao ligi itakuwa ngumu kwa sababu timu nyingi zimesajili na zimejiandaa, nafikiri ni jambo la kusubiri kuona nini kinatokea lakini ni jambo jema kujiandaa vizuri mapema,” amesema Kagoma.
Naye Afisa Habari wa timu hiyo, Hussein Masanza amesema baada ya kumaliza kambi jijini Arusha timu itarejea Singida kwenye tamasha litakalotumika kutambulisha wachezaji wapya pamoja na wale wanaoendelea.