Kiungo Mshambuliaji wa Simba SC Yusuph Mhilu amesema kuna uwezekano mkubwa akarudi Kagera Sugar kwa Mkopo, kufuatia kufikia makubaliano binafsi na Klabu hiyo.

Mhilu alisajiliwa Simba SC mwanzoni mwa msimu wa 2021/22, lakini ameshindwa kuonyesha kiwango, na kujikuta akiwekwa kwenye orodha ya wachezaji watakaoondoka kwa Mkopo, katika kipindi hiki cha usajili kuelekea 2022/23.

Mhilu amesema Uongozi wa Simba SC ulimpa nafasi ya kutafuta timu, ambayo ataichezea kwa Mkopo kwa msimu ujao, na kwa sasa amefanikiwa kuishawishi Kagera Sugar ambayo ameitumikia kwa kipindi kirefu kabla ya kutua Msimbazi.

Amesema mbali na Kagera Sugar, pia alipata nafasi kwenye klabu ya Kwambwe Worrious ya Zambia, lakini dili hilo limeshindikana, kutokana kushindwa kufikia makubaliano binafsi.

“Nilipewa nafasi ya kutafuta timu ambayo naweza kucheza kwa mkopo. Kulikuwa na timu mbili ya Kabwe Warriors ya Zambia na waajiri wangu wa zamani Kagera Sugar, hivyo nimeamua kurudi nyumbani kutokana na kuelewana maslahi tofauti na Kabwe,”

“Kagera ndiko nilikokulia kisoka na walinipa nafasi ya kuonekana hadi Simba kunisajili, hivyo nina uhakika wa nafasi ya kucheza kwa mara nyingine nikiwa huko na ninaahidi kuitumia ipasavyo ili kurudi kwenye kiwango changu cha mwanzo, sitaki kufanya makosa.” amesema Mhilu

Kagera Sugar imejizatiti kufanya usajili wenye kiwango chini ya Kocha Mkuu Francis Baraza, na tayari imeshatangaza kuwatema wachezaji kadhaa ili kukifanyia maboresha kikosi chao kuelekea msimu mpya wa 2022/23.

Mandela ndani ya mioyo ya Mataifa Ulimwenguni
Serikali matatani kwa kuwabagua Ogiek