Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera amefunguka kuwa wapinzani wao Pyramids wako juu kuliko wao ambapo hawezi kulalamika kwa matokeo ambayo waliyapata walipokutana nao katika Kombe la Shirikisho Afrika.
Zahera Jumapili iliyopita alishuhudia kikosi chake kikikubali kipigo cha mabao 2-1, mbele ya Waarabu Pyramids katika mchezo wa kusaka nafasi ya kutinga hatua ya makundi ya Kombe hilo la Shirikisho Afrika.
Kwa sasa Yanga wanajiandaa na mechi ya marudiano dhidi ya Pyramids ambayo itapigwa nchini Misri Novemba 3, huku wakihitaji ushindi wa mabao 2-0 kwa ajili ya kusonga mbele.
Zahera raia wa DR Congo, amesema kuwa hawezi kulalamika kwa ajili ya matokeo ambayo wameyapata kutoka kwa wapinzani wao kutokana na ukweli kuwa wapinzani wao wako juu kuliko wao.
“Hii ni kama bahati mbaya ya kupoteza mchezo huu kama ambavyo ilitutokea kule Zambia tulipocheza na Zesco.”
“Ukiangalia mabao ambayo wameyapata ni kama yale ya mchezo uliyopita na Zesco lakini hatuwezi kulalamika sana.”
“Wengi wanalalamika kwa sababu tulibadilisha uwanja lakini niwaambie mabadiliko haya wala hayajatuathiri kwa kitu chochote kile.
“Ukweli ni kuwa wenzetu wako juu kuliko sisi na hilo liko wazi na hatuwezi kulalamika kwa sababu wametufunga, kitu cha muhimu ni kuangalia mechi ya pili tutafanya nini,” alimaliza Zahera ambaye anatajwa kuwa anaweza kutimuliwa kwenye timu hiyo.