Kikosi cha Coastal Union kinaendelea kujifua kujiandaa na Ligi Kuu Bara inayoanza kesho Jumanne (Agosti 15), huku kocha wa timu hiyo, Mwinyi Zahera akimtega Ibrahim Ajibu akitaka kumpa unahodha kama alivyofanya walipokuwa Young Africans misimu mitano iliyopita.

Uamuzi huo umeelezwa kuwashtua baadhi ya Wananmangushi kutokana na ukweli Ajibu ni mgeni katika kikosi hicho, lakini Zahera amesema nyota huyo wa zamani wa Simba SC, Young Africans, Azam FC na Singida Big Stars ana vitu vinavyombeba kupewa nafasi hiyo.

Ajibu mwenye umri wa miaka 26, amekuwa akifanya makubwa uwanjani kwa ujuzi wa kumiliki mpira, kupiga pasi za mwisho za mabao ya kideoni, lakini ameshindwa kuwa kwenye kiwango tangu alipoachana na Zahera na kurejea Msimbazi.

Zahera amesema “Ibrahim Ajibu ana mchanganyiko wa vitu vingi ikiwemo talanta (kipaji). kujitolea na ukomavu wa miaka mingi. Ameonyesha sifa za uongozi na anafaa, pia naamini ni wakati wa kuonyesha uwezo wake akiwa kama nahodha,” amesema Zahera.

Ajibu mwenyewe alipoulizwa juu ya taarifa za kupewa tena kitambaa, alishukuru kwa kusema; “Ni heshima kubwa ya kuchaguliwa kuwa kiongozi wa wenzako na mtetezi wao. Nimekuwa nikijitahidi kuongoza kwa kuonesha mchango mzuri wa mafanikio ya timu. Ikiwa nimepewa fursa, nitafanya kazi nzuri ya kuhamasisha wenzangu na kuwaongoza kwa ushindi.”

Hata hivyo, Ajibu atalazimika kufanya kazi ya ziada kwani tangu alipoondoka Young Africans mwaka 2019, hajarejea kwenye makali yake na kupewa kitambaa hicho kwake itakuwa ni kama mtego ambao lazima autegue kutuliza nyoyo za Wanamangushi walioanza minong’ono mapema kutokana na sifa za uvivu zinazodaiwa kuwa nazo kiungo huyo mshamnbuliaji.

Katika hatua nyingine, timu hiyo imeendelea kufanya usajili ikiwa mbioni kumalizana na mshambuliaji Mkongo, Henock Mayala, aliyekuwa akikipiga Polisi Tanzania iliyoshuka daraja msimu uliopita sambamba na Ruvu Shooting na Mbeya City.

Mbali na Mayala, pia Coastal imemalizana na Mcrotia Fran Golubic aliyepewa mkataba wa miaka miwili.

“Tunamalizia malizia kusajili sasa, kwa wachezaji wa ndani ambaye bado hajasaini ni Mapinduzi Balama ingawa tumefarnya naye mazungumzo tayari,” kimesema chanzo hicho.

Coastal hadi sasa imesaini wachezaji sita akiwamo Ibrahimn Ajibu, Ally Kombo (Ruvu Shooting), Lucas Kikoti (Namungo FC), Abdallah Denis (Malindi), Dennis Modzaka (Bechem United), Abdulswamad Kassin (Geita Gold).

Kambi upimaji Afya, matibabu kuzinduliwa Tanga
Shambulio la anga lauwa raia 70 wakiandamana