Aliyekua Kocha wa Young Africans Mwinyi Zahera amesema anaamini kujiamini na utayari wa Wachezaji wa Simba SC ndio sababu kubwa ya klabu hiyo kufanikiwa kufuzu hatua ya Makundi mara nyingi zaidi ya klabu nyingine yoyote Tanzania na Afrika Mashariki.
Simba SC imetinga hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika mara ya tatu ndani ya miaka mitano, hali ambayo imedhihirisha ukubwa wa klabu hiyo kutoka nchini Tanzania.
Akizungumza kupitia Kipindi cha Sports HQ cha EFM Radio, Zahera amesema imefika wakati wachezaji wa Simba SC wameshaweka akilini mwao kuwa kutinga hatua ya Makundi ni jambo la kawaida na imewasaidia kwa kiasi kikubwa.
Amesema jambo hilo ni tofauti na wachezaji wa klabu nyingine za Tanzania ama Afrika Mashariki, huku akisisitiza hadi kufikia hatua hiyo kuna kazi kubwa imefanywa na viongozi kwa kushirikiana na wadau wa klabu hiyo yenye maskani yake makuu mtaa wa Msimbazi-Dar es salaam.
“Kwa sasa wachezaji wa Simba SC wameshajiwekea akilini kuwa, kuingia hatua ya Makundi ni jambo la kawaida kwao na ndio maana wanacheza wakijiamini hata wakutane na timu ya aina gani, hii ni tofauti sana na klabu nyingine za hapa Tanzania ama Afrika Mashariki kwa sasa,”
“Hata katika maisha ya kawaida ukishajiamini kwa kufanya jambo kubwa na kulirudia kila siku hauwezi kufeni hata mara moja, ndivyo ilivyo kwa Simba SC, kwa hiyo wamepiga hatua na wana kila sababu ya kufanikiwa katika mpango wa kusonga mbele kwenye Michuano hii ya Afrika.” amesema Zahera
Akiwa Kocha Mkuu wa Young Africans Zahera aliwahi kujaribu kuifikia Hatua ya Makundi Young Africans msimu wa 2019/20, lakini alishindwa baada ya kikosi chake kutolewa na Zesco United ya Zambia kwa kufungwa jumla ya mabao 3-2.
Alipoangukia Kombe la Shirikisho, pia hakufanikiwa baada ya kukutana na kisago kutoka kwa Pyramid ya Misri, ambapo Young Africans ilipoteza nyumbani 1-2 kabla ya kwenda ugenini na kupoteza kwa 3-0.