Aliyekua kocha wa Young Africans Mwinyi Zahera amesema hawezi kuifundisha klabu ya Township Rollers ya Botswana, kwa kuwa hawezi kuzungumza vizuri kiingereza.
Zahera ambaye alitimuliwa Young Africans Novemba 2019 kufuatia mwenendo mbaya wa matokeo, amesema amefanya mawasilino na wakala wa Botswana ambaye alimuarifu kuhusu mpango wa Township Rollers kusaka kocha.
Amesema wakala huyo alimuona wakati akiwa na kikosi cha Young Africans, pindi timu hizo zilipokutana kwenye michuano ya kombe la shirikisho mwanzoni mwa msimu huu wa 2019/20.
“Nimepigiwa simu na wakala kutoka nchini Botswana akinieleza kwamba klabu huyo inatafuta kocha na kusema kwamba vile nalikwenda kule na Yanga ndio wale viongozi wawo walinanii..waliniona.” amesema Zahera.
“Tukasalimiana na huyo wakala, nikamueleza kwamba siwezi kwenda Botswana kwa sababu siwezi kuzungumuza kingereza, kwa hiyo itakuwa shida kwangu kuenda kule.”
Hata hivyo kocha huyo kutoka DR Congo ametanabaisha kuwa, tayari ameshapata ofa tatu, na anaendelea kufikiria wapi anapaswa kwenda kuanza kazi yake ya ukufunzi wa soka.
“Kwa sasa nina ofa kutoka kwenye timu tatu, zimeonyesha nia ya kutaka kufanya kazi na mimi, ninaendelea kufikiria, nikifanya maamuzi sahihi nitaweka wazi ninapokwenda kuendelea na majukumu ya kufundisha soka.”
Zahera alijiunga na Young Africans Mei 2018 akichukua nafasi ya Mzambia, George Lwandamina, na alifaniiwa kukiongoza kikosi cha klabu hiyo hadi kumaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kuu msimu wa 2018/19.