Mkurugenzi wa Idara ya Utalii kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Zahoro Kimwaga amesema kuwa sera na miongozo inayoongoza sekta ya utalii imepitwa na wakati kutokana na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii yaliyotokea.
Ameyasema hayo wakati wa warsha ya siku moja iliyoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii ya kuwakutanisha wadau wa sekta hiyo Nyanda za Juu Kusini ili kukusanya maoni yao kuhusu upungufu wa utekelezaji wa sera hiyo ambayo kwa sasa imeonyesha kutokuwa na tija.
’’Si hayo tu sera ya awali haikuainisha vivutio vyote vya utalii zaidi ya hifadhi pekee ambapo kwa sasa tatizo la ujangili na mabadiliko ya tabia nchi yameathiri kwa kiasi kikubwa,’’ amesema Kimwaga.
Amesema kuwa Sera mpya itakayoundwa itaweza kwenda sambamba na aina ya utalii wa sasa ambao kipindi cha nyuma haukuwepo, huku akitolea mfano utalii mikutano pamoja na utalii wa kiutamaduni ambao umekuwa ukikua kwa kasi hapa nchini
Hata hivyo, ameongeza kuwa wanahitaji miongozo mipya itakayosimamia sekta hiyo ili kuondoa migongano ya kiutendaji katika taasisi zinazohusika ikiwemo ya wanyamapori, misitu na uwekezaji ili kuendeleza utalii nchini.