Shirika la Viwango nchini Uganda (UNBS) limesema kuwa limebaini zaidi ya nusu ya bidhaa zilizo kwenye soko la nchi hiyo ni feki au viko chini ya kiwango.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na shirika hilo mwezi Februari, umebaini kuwa takribani asilimia 54 ya bidhaa zilizoko kwenye soko la nchi hiyo hazikukidhi kiwango kilichowekwa, hivyo kuwa katika hatari zaidi ya kuwa feki.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji Msaidizi wa Ukidhi wa Sheria – UNBS, Paul Musimami amesema kuwa asilimia hizo zimeshuka kutoka asilimia 80 iliyokuwepo miaka mitano iliyopita. Amesema kupungua kwa asimilia za bidhaa feki kumetokana na jitihada za Shirika hilo kwa kushirikiana na wadau wake.
“Utafiti wetu uliofanywa Februari umebaini kuwa zaidi ya asilimia 54 ya bidhaa zilizoko sokoni hazijakidhi viwango. Kwa bahati mbaya sehemu kubwa ya bidhaa hizi ni zile zilizotengenezwa hapa nyumbani,” alisema Musimami.
“Tumezuia bidhaa nyingi zilizokuwa zinaingia na ambazo zilikuwa kwenye mpango wa kuingizwa nchini kwa kutumia program ya uthibitishaji,” aliongeza.
Kwa mujibu wa ripoti ya Standard Bank Group, bidhaa zisizokidhi viwango nchini humo ni tatizo kubwa linalokabili uchumi likiigharimu nchi hiyo zaidi ya UGS 1 trilioni.
Musimami alieleza kuwa sehemu kubwa ya bidhaa hizo ni vifaa vya umeme, samani na chakula. Pia, alitaja vifaa vya maliwatoni pamoja na baadhi ya vipodozi.