Zaidi ya wafungwa 200 wametoroka jela katika wilaya ya Moroto, kaskazini mashariki mwa Uganda na kukimbilia kusikojulikana jambo lililosababisha watu katika mji huo kuacha shughuli zao wakati askari wakijaribu kuwarudisha wafungwa hao.

Msemaji wa Idara ya Magereza ya Uganda, Frank Baine amesema wafungwa hao walitoroka jela jana Jumatano, baada ya baadhi ya wafungwa hao kuwafyatulia risasi askari waliokuwa wanawalinda.

“Kumejiri tukio la kutoroka jela. Tungali tunajaribu kukusanya taarifa juu ya tukio hilo sanjari na kuwabaini wafungwa waliotoroka,” amesema Baine.

Baine amesema, wafungwa saba wamekamatwa tena na watatu wameuawa, na vikosi vya jeshi la magereza, jeshi la ulinzi na polisi vinashirikiana kwa pamoja kuwakamata wafungwa waliotoroka.

Bila kutaja idadi kamili, amesema idadi ya wafungwa waliokimbia jela ni kubwa mno, wengi wakiwa wamehukumiwa kutokana na kumiliki isivyo halali silaha za moto, wamechukua bunduki 15 na risasi kadhaa wakati wanatoroka.

Kadhalika ametoa mwito kwa wafungwa hao kujisalimisha kwa taasisi husika na kueleza bayana kuwa, maafisa usalama wakiwemo wanajeshi na askari polisi wanawasaka wafungwa hao ili kuwakamata tena na kuwarudisha jela.

Itakumbukwa kuwa, Machi mwaka huu, wafungwa watatu waliuawa huku wengine sita wakijeruhiwa katika jaribio jingine la kutoroka gerezani katika wilaya ya Arua, kaskazini magharibi mwa Uganda.

KMC FC yaifuata Mwadui FC
Young Africans yawasili Bukoba